mwanakheir

Mwanakheir Ahmed Abdul Rahim Mahmoud

Dactari

MIMI NI NANI?

Mimi nimezaliwa Zanzibar lakini pia nna asili ya Comoro ambako mamaangu na familia za upande wa babaangu zinakotoka. Aidha, vizazi viwili upande wa babaangu ni wazaliwa wa hapa Zanzibar. Mimi ni mama. Nna mtoto mmoja wa kike ambaye ana watoto wawili. Nnashukuru na nna furaha kuwa mimi. 

Kuwa karibu na watu, kuwa na mahusiano na wengine.

Ni muhimu sana kuwa karibu na watu na kuwa na mahusiano na watu. Kwa kweli, nahisi kila mtu anahitaji kuwa na mahusiano na binaadamu mwengine.

Familia

Mimi nahisi, familia ni kitu muhimu sana katika maisha. Kuna umuhimu sana kila mmoja kujali na kuwa karibu na mwenziwe. Unapojisikia una familia iliyo na furaha, hapo ndipo unapoweza kuwa imara na kuwa na mchango mkubwa katika maisha. Unaweza kufanya mambo mengi ya maana katika dunia. Kwangu mimi familia ni kitu muhumu sana na ni cha kukipa kipaumbele. Ni muhimu kuwa na msingi mzuri wa kujijenga kimaisha. Hata kama unafanya chochote kinachokuhusu wewe binafsi, ni vizuri pia kuifikiria familia.

Kazi kwa ajili yangu na wengine

Kwangu mimi ni muhimu sana kufanya kazi kwa uwezo wote mtu alionao. Kwani ukifanya kazi nzuri itakupa faraja wewe, familia yako na unaowafanyia kazi. Hii ni kwa kazi ya aina yoyote ile. Ni vigumu sana kupata furaha iwapo jamii inayokuzunguka haina furaha kutokana na dhiki zinotokana na umaskini. Itakuathiri tu hata uwe na kipato cha aina gani. Huwezi kuwa na amani katika maisha. Mazingira yana mahusiano makubwa na maisha yako. Kama kuna mambo mabaya katika mazingira yako, kama vile usumbufu, vurugu, ubakaji, wizi, hautakuwa na amani. Ni shida kubwa. Ntakuwa na furaha na amani iwapo jamii ilonizunguka ina furaha na imeridhika kimaisha.   

Kujitunza

Siku hizi watu wa Zanzibari hawatunzi sana miili yao kama zamani. Miaka ya nyuma watu walitunza sana miili yao. Ilikuwa desturi wanawake kwenda kusingwa na kukandwa, kupaka hina na kusuka. Siku hizi watu wamekuwa na harakati nyingi. Kila mtu anatafuta malengo ya kukimu maisha. Watu wanafanya kazi sana, bila kujali miili yao.

Usipoteze upendo

Kwa kijumla, siku hizi mapenzi yamepungua. Labda sio kila mahali katika dunia, lakini kwa mfano hapa Zanzibar watu walikuwa wanaishi kwa karibu na kila mmoja alikuwa anamjali mwenziwe bila kujali itikadi za kisiasa au dini. Kulikuwa na amani sana na imani. Watu waliaminiana na kupendana sana. Hivyo ndo mimi nnavyohisi. 

– Nini kilitokea?

Sijui. Hivi sasa jamii ya Zanzibar imegawanyika wakati huko nyuma kila mtu katika jamii alimjuwa mwenziwe kwa wema kama mfano wa familia kubwa. Hii yote ilitokana na kuaminiana na uwepo wa mahusiano mazuri ya watu katika jamii. Siku hizi hata majirani si aghlabu kusaidiana katika shida na matatizo. Kwa kweli jamii imesambaratika….. sijui niliezeje. Watu wengi wamegawanyika kuliko kuwa pamoja. Watu wanazungumzia zaidi tofauti zao kuliko upendo na mshikamano baina yao. Tukiendelea hivi, itatuathiri sisi na vizazi vijavyo. Nafikiri kuna haja ya kuelemishana sana katika jamii juu ya kupendana na kuishi kwa amani na kuelimisha juu ya haki za kijamii na kijinsia. 

Tuache kupenda makubwa

Siku hizi watu wanapenda makubwa kuliko zamani. Wanafanya kazi sana kuongeza kipato kuliko kujali mahusiano ya kifamilia. Mimi nafikiri watu wanajali zaidi kipato kuliko familia na jamii. Ingawa kuna wanofanya kazi sana ili waweze kumudu maisha, lakini wengi wanataka kipato zaidi ili waishi maisha ya kifahari kwa kujilinganisha na wengine. Kwangu mimi, cha muhimu ni kuishi maisha ya wastani ambayo yatakidhi mahitaji yangu muhimu na mara moja moja kwenda kujipumzisha katika sehemu nzuri ambako si lazma kununua chakula au kinywaji cha bei ghali. Chakula kizuri na gilasi ya kinywaji cha “juice” kinaweza kuniridhisha. Pia napenda mara moja moja kusafiri na familia kwa mapunziko. Hayo ndo mahitaji yangu ya msingi kimaisha. Mimi nahisi, kujilinganisha na wengine kusiwe ndo kigezo cha sisi kuendelea kupanda juu kimapato. Kila mmoja anahitaji kutosheleza mahitaji yake mwenyewe ya msingi na kuridhika. Natafuta neno zuri. Nachomaanisha ni kwamba hata tuwe na kingi kiasi gani, bado tunataka zaidi na zaidi.

Ndoto

Kama utakuwa unaishi kwa desturi isiyo na mabadiliko, si rahisi kuendelea kimaisha. Kuishi ni kuwa na uwezo wa kupata na kufanya yale unayoyapenda na kufikia ndoto yako. Kadri ya unavyofurahi, basi maisha yanaendelea kuwa mazuri. Aidha wako watu ambao ni maskini lakini wana furaha kwa vile wameridhika na kukinai hali walizonazo. Wameridhika kubaki katika hali hizo ilimradi tu wanapo pa kukaa, wana familia, na waweza kupata chakula. Hata hivyo wapo maskini ambao pia huwa na ndoto na kujaribu kuzifikia ndoto zao ambazo hupelekea wao au jamii zao kuendelea kimaisha. Ili uweze kukuwa na kuendelea kimaisha, ni muhimu kuwa na ndoto. Lakini inapokuwa ndoto yako ni ya kutaka ufakhari au kujilinganisha basi maisha yanaweza kuwa magumu. Bila shaka, cha msingi ni kuwa….. mimi naamini furaha inatokana na kupata au kifikia kile ambacho “nafsi” inakipenda na kukifurahia.

Join us … travelling and discovering culture, people and yourself