
Musini Shauri Hadhi
Mganga wa Tiba za Asili
MIMI NI NANI?
Mimi ni mganga wa tiba za asili niliyejifunza maarifa haya ktoka kwa mababu zangu. Niliyapata kutoka kwa wazazi wangu. Nilifundishwa nao na nimedhamiria kurithisha maarifa haya kwa watoto wangu. Mbali na kazi hii, naishi maisha ya kawaida kama mkulima.
Kufanya kazi maishani
Ni muhimu kufanya kitu maishani mwako, kufanya kazi. Kuwasaidia watu, kuwa na afya njema na kufanya kilimo. Kazi na kujituma ni nguzo muhimu za maisha. Kufanya kazi ni moja ya maadili ya msingi zaidi maishani.
Mahusiano kati ya watu. Kuishi pamoja
Wazanzibari ni watu wenye ukaribu sana. Kwetu sisi mahusiano kati ya mtu na mtu ni jambo muhimu; kuwa pamoja, kuishi pamoja, kufanya kila kitu pamoja, kula chakula pamoja na kutumia muda pamoja. Pale mtu anapofariki au anapooa, ni muhimu kuwaalika majirani na wapendwa ili kuwa pamoja katika nyakati kama hizo, ili kushirikiana pamoja, alikaneni. Katika utamaduni wa Zanzibar, maneno ya uchangamfu na ukarimu “Karibu”, “Kaa kitako”, “Chai” (Karibu kwangu, kaa kitako, pumzika, kunywa chai) ni ya muhimu. Familia inapaswa kufanya kazi pamoja na kusaidiana. Mume anapaswa kumsaidia mke wake, mke amsaidie mume, na watoto nao pia wanapaswa kusaidia. Tabia njema na kuheshimu wengine ni muhimu maishani. Wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto wao tabia njema na maisha mema. Hapo kiwango cha uhalifu, ukahaba au ukatili kitashuka.
Kudumisha utamaduni wako
Ni muhimu kudumisha utamaduni wako. Vijana wengi wa Kizanzibari wanajaribu kuiga tabia za Ulaya na kuhamishia hapa mitindo ya kule. Kwa mimi ni muhimu, na najivunia, kwamba familia yangu inaishi kulingana na desturi na inazingatia kanuni za desturi za kimwenendo, mila zetu, na kuvaa kitamaduni. Vivyo hivyo, tunakula kitamaduni kwa kutumia mikono yetu na tunakula vyakula vya kitamaduni. Wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto wao utamaduni wao nyumbani.
Kuendelea kuishi. Usalama
Maishani ni muhimu kuwa na uwezo wa kuendelea kuishi; kuwa na kitu cha kula na kuwa na fedha ya kununua chakula. Usalama ni muhimu, unapoukosa, huwezi kuwa na furaha. Kamwe huwezi kuwa na furaha kama una hofu.
Elimu
Watoto inabidi waende shule ili waweze kujifunza. Watakapojifunza, wataweza kupata kazi na kujipatia kipato. Tunapaswa kutenga muda kwa ajili ya watoto na kuwaelimisha ili waweze kuwa na maisha mazuri. Kwa kufanya kazi, wataweza kufurahia maisha yao yajayo.
Nyumba
Ni muhimu kuwa na familia na kuweza kujenga nyumba kwa ajili familia. Kwa mimi, furaha ni kutumia muda wangu pamoja na familia yangu yote wakati wa kuhitimisha Ramadhani. Familia yote inapokutana, chakula kinapikwa – pilau. Watoto, watu wazima, ndugu na marafiki wote wanakula pamoja. Kunakuwa na watu tofauti-tofauti, tunakutana pamoja ili kuonesha sisi sote ni sawa.
Fedha
Fedha ni muhimu kwa sababu ukiwa nayo unaweza kununua chakula.
Kufurahia maisha
Ni muhimu kufurahia maisha.
– Baadhi ya watu wana fedha, wana vitu vingi lakini hawana furaha.
Inategemea na mtu na nini anachokitaka maishani. Hatujui moyo wa mtu fulani unataka nini hasa. Mara nyingi mtu hajui moyo wake unataka nini ili awe na furaha.
– Je, moyo wa mwanadamu unataka nini?
Kama una fedha nyingi, kwanza tazama marafiki, kama kuna yeyote anayehitaji msaada, msaidie. Tazama familia yako, je wapo watu wanaohitaji msaada, wagonjwa? Wasaidie, nunua dawa, na watembelee hospitalini. Hii itakuwa chakula kwa moyo wako.
– Je, unapataje furaha?
Ushauri wangu ni kuwasaidia watu wengine wanaohitaji msaada. Na mwamini Mungu au Allah. Kwa mimi, furaha ni kila kitu kinachonipa faraja maishani. Mungu anatupatia kile hasa tunachohitaji. Anatufundisha kile tunachopaswa kufanya ili tuendelee kuishi. Anatutunukia siku. Hata kama hatuna pesa, au hata kama tunayo kidogo sana, anatupatia fursa ya kuiona siku na anatupatia kiasi cha kutosha kuendelea kuishi siku inayofuata. Anatupatia faraja kila siku inayopita. Nafurahi pale ninapoamka kila asubuhi na kila kitu kinachonizunguka kipo sawa; kwamba familia yangu ina furaha, na kila kitu kwenye familia kinaenda vizuri. Kama nitakuwa na imani kwamba Allah atalishughulikia jambo fulani, nitapokea kila kitu ninachohitaji ili niishi. Hakikisho hili ndilo linalonipa furaha. Iwapo nitaamka na kujihisi mgonjwa au pale familia yangu inapoumwa, basi hilo haliwi jambo jema. Hapo sitakuwa na furaha.
Afya
Kwa sasa watu hawali kile wanachopaswa kula, hawajidhibiti; hii ni tabia inayoharibu mwili na pia inawafanya washindwe kufurahia maisha kikamilifu. Watu wanaotaka kuishi kwa furaha wanapaswa pia kula kwa usahihi huku wakizingatia kujidhibiti. Mwanadamu anapaswa kula kile kinachoota kwenye mazingira yake. Hapa tunakula viazi, mihogo na ndizi. Dawa za asili zitaendelea kuwepo duniani kote. Hapo zamani za kale, watu walitumia dawa za asili na ziliwasaidia na walikuwa wenye afya njema. Hivi sasa watu wanatumia dawa zenye kemikali na matatizo yanaanza kujitokeza. Ningependa kusema kwamba wanapaswa kutumia mitishamba itakayowapa afya njema na hisia ya furaha.