musa

Musa Makame Musa

Sheha – Kiongozi wa kijiji 

MIMI NI NANI?

Jina langu ni Musa Makame Musa. Nina miaka 71. Nina watoto nane, mabinti 5 na wana 3. Nilizaliwa katika kijiji hiki cha Kibeni na naishi hapa hata hivi leo. Mimi ni kiongozi wa kijiji kwa miaka 15, ambapo watu 3,300 wanaishi.

Jijali wewe mwenyewe, kwa ajili ya afya yako. Tumezaliwa ili tuwe na maisha mazuri na yenye furaha

Pale watoto wanaponiuliza maisha yanahusisha nini hasa, nawaambia kwamba inabidi wajali afya zao. Sijawahi kamwe kuvuta sigara kwa miaka 71 na sijawahi kunywa pombe. Situmii vitu vyovyote vyenye kemikali. Watoto wangu wote wananifuata. Hakuna kati yao anayevuta sigara, anayekunywa pombe au kutumia vichocheo vyovyote. Hii ni asili yao, asili ya makuzi yao. Vijana wanakunywa pombe kwa sababu familia zao hazikufanya vizuri, hazikuwa makini, hazikuwaangalia walipokuwa makinda, walipokuwa wakikua. Kisha wataondoka nyumbani ili watafute uhuru ili kwamba asiwepo mtu wa kuwadhibiti. Kisha wanakutana na watu tofauti wanaopendekeza starehe mbalimbali, wanawashawishi kunywa pombe. Kijana anaaza kunywa. Anarudi nyumbani akiwa mraibu. Hana tena nguvu ya kufanya kazi. Pombe imechukua nguvu zake zote. Kwa mimi hata kama kijana wa kiume ni mtu mzima, si vyema kwamba aenende kwa namna hiyo. Pia kwa niaba ya mahusiano ya mama na mwana na mama na binti. Sikubaliani na tabia hiyo. Tumezaliwa ili tuwe na maisha mazuri na yenye furaha. Tuwe na afya njema. Kama tusipozingatia afya zetu, inamaanisha kwamba hatutaki kuishi vizuri na kwa furaha. Kama una afya njema, unaweza kuwa tajiri, unaweza kusoma, unaweza kufanya chochote utakacho maishani mwako. 

Fanya kazi pia ili usaidie wengine

Tunapaswa kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maisha yetu. Kama hufanyi kazi kwa bidii, huna maisha mazuri. Kisha tamaa ya kuiba inazaliwa. Jambo gumu kukubaliana nalo, nisilolipenda, pale watu wanapokunywa pombe, vichocheo, iwapo unakunywa kupita kiasi, unapoteza maisha yako, unapoteza fursa ya kufanya kazi. Kisha unaanza kuiba. Ningependa watoto wasome ili waendeleze maisha yao. Mimi nina miaka 71 lakini bado naonekana kijana, kwa sababu daima nimekuwa nikifanya kazi, nafanya sana kazi na bado naendelea kufanya kazi. Napenda kufanya kazi. Labda ndiyo maana Mungu ananipa afya na mwonekano wa ujana. Yawezekana pia kwa sababu nilizaliwa ili kusaidia wengine. Nilianza na shule, kujenga shule na barabara. Najaribu kusaidia watu katika kila hali. Mimi si tajiri. Ni mwajiriwa mwenye mshahara. Mshahara wangu si mkubwa. Nina shamba langu. Mimi si tajiri lakini daima, iwapo mtu anakuja kwangu, nitagawana nae kile nilichonacho.

Heshima huanzia nyumbani

Inakubidi uwaheshimu watu wote duniani. Watu wote utakaokutana nao  maishani mwako. Hii ni muhimu tangu mwanzo kabisa. Ni muhimu kwa wazazi kuwafundisha watoto kuheshimu wengine. Inaanza kwa kujifunza kuheshimiana kuanzia nyumbani. Heshima kwa baba na mama yangu. Lakini pia wazazi ni walimu wa kwanza wa heshima, namna wanavyoheshimiana wao wenyewe. Heshima ni kipengele cha utamaduni wetu. Huu ni utamaduni wa Wazanzibari. Lakini ukirudi nyuma katika historia, hapo zamani utaona kwamba heshima inaongelewa kwenye kila dini, Uislamu, Ukristo au dini yoyote ile. Hiki ni kipengele cha utamaduni wetu wa kibinadamu. Ukosefu wa heshima unaharibu utamaduni na dini. 

Jifunze kwa ajili ya siku zako za usoni zilizo njema

Watu wote wanapaswa kupata elimu na kujifunza. Kwa sasa nina mabinti wawili ambao bado hawajaolewa. Mmoja amefikia sekondari ngazi ya juu na mwingine amesoma Chuo Kikuu cha Zanzibar. Ningependa waendelee na masomo na kupata maarifa. Maarifa ni kwa ajili ya kila mtu, ni mustakabali na hazina. 

Famila inayoshikamana hujaa upendo

Kinachonipa furaha ni kuona watoto wangu wote, mabinti na wana wote wakiwa wameketi pamoja. Wanapendena wao kwa wao na wanawapenda mama na baba yao. Kwa hilo nahisi furaha sana. Familia yangu bado inakaa pamoja, pembeni ya nyumba ya baba na mama yangu, kuna nyumba za ndugu zangu, na watoto wao. Tunakula chakula pamoja, tunasaidiana. Lakini hii si kila mahali. Kwa sasa hata familia hazishikamani kutokana na tofauti za kisiasa. Natamani katika maisha yangu yote kwamba familia yangu iwe pamoja baada ya kifo changu. Kutafuta njia ya familia yote kuwa pamoja na kusaidiana. Hivi leo ninapoona kila mtu ameketi pamoja, najivunia. Kuanzia leo ningependa kukualika kwenye familia yangu. Utakuwa mmoja wetu. Hutakuwa peke yako. Nyumba yangu i wazi kwako, wakati wowote unapotaka kuja. Daima tutakukaribisha. Hapa ni nyumbani kwako. Kama utaomba msaada, daima tutakusaidia. Iwapo utarudi Ulaya, unaweza kuchukulia kwamba una familia yako hapa Zanzibar.

Join us … travelling and discovering culture, people and yourself