
Mariam Mohammed Habdan
Mwanamuziki – Mwandishi wa habari
MIMI NI NANI?
Mimi ni mwanamke mwenye miaka 75 lakini najihisi kama mwanamke wa miaka 25. Ningependa kufanya mambo mengi zaidi na kusaidia watu wengi. Mimi ni mwanamke mwenye furaha. Napenda muziki, napenda dini, nampenda kila mtu. Naheshimu hisia ya upendo iliyo ndani yangu. Simwonei wivu mtu yeyote. Nashukuru kwa kila kitu kilichotokea maishani mwangu. Namshukuru Mungu na namshukuru kila mtu. Huu ni msimamo wangu mpaka siku nitakayokufa.
Kukua pamoja kwenye jumuiya. Vizazi vinapaswa kuwa pamoja
Zamani, kila mtu alikuwa akicheza pamoja na wavulana na wasichana. Sasa hivi nioneshe eneo ambalo watoto wanaweza kucheza. Sasa hivi tunazo sehemu zinazoitwa viwanja vya michezo ya watoto, ambapo wanakwenda na wazazi wao. Wazazi wanasubiri na kwa kawaida watoto wanacheza peke yao na wanakula peke yao. Zamani kulikuwa na maeneo ya kucheza mbele ya nyumba, si kama sasa. Kulikuwa na michezo mingi iliyowaunganisha watoto na kutengeneza udugu. Watoto waliishi karibu pamoja kwenye jumuiya iliyoundwa na Wahindu, Wabohora, Washirazi, baadhi walitoka Comoro. Wote walicheza pamoja. Jambo hili halipo hivi sasa. Kwenye kila eneo la wazi kuna mradi unaendeshwa, majengo ya makazi yanajengwa. Na hilo ndilo tatizo. Mama yangu aliponiita, wazazi au wanawake wengine walinifahamu mimi ni nani na wapi nilipo. Kila mtu alimfahamu mwenzake. Isingewezekana nipite bila kutambulika. Kila mtu aliuliza: ”Unakwenda wapi?”. Watu wazima wote walilea watoto wote. Hivi sasa maisha yamebadilika kabisa kwa watoto, kwa wazazi, na kwa jumuiya. Sijui hata nisemeje. Kama nikisema jambo fulani limebadilika na kuwa zuri au baya, basi kila mtu atakuwa na maoni tofauti kwa sababu inategemea na jinsi watu wanavyoyatazama haya mabadiliko. Tuna simu na intaneti zinazotushughulisha, zinazoshughulisha akili zetu. Lakini kwa upande mwingine, runinga au redio si lazima ifunguliwe siku nzima. Tunaweza kuchagua. Maisha ya kifamilia nayo yamebadilika. Tulizoea kuishi pamoja na bibi, mama na akina shangazi ndani ya nyumba moja. Nyumba ilikuwa na vyumba 3 au 4 vya kulala. Kwenye chumba kimoja bibi alilala na shangazi na wasichana wachache. Wavulana walilala kivyao. Watoto walikuwa chini ya uangalizi wa wakubwa wakati wote, ambao waliangalia jinsi watoto wanavyoenenda na kuwalinda. Kisha, kama watoto, tulizoea kuadhibiwa na wazazi, lakini tulijifunza mengi. Nyumbani tulijifunza mengi kutoka kwa mabibi na mama zetu. Pia kwa wasichana, Somo alikuwa mtu muhimu sana. Somo ni “Mama wa dhahabu”. Aliwafundisha wasichana wanachopaswa kufanya na wasichopaswa kufanya, walichoruhusiwa kufanya na wasichoruhusiwa kufanya, pia katika masuala ya mahusiano na mwanaume. Hivi sasa nani anafundisha jambo hili? Wapo wapi Somo?
Wajibu wa wazazi, kina mama na watoto. Wajibu wa kina baba kwa familia
Zamani, kina mama waliweka mkazo mkubwa kwa malezi ya watoto, hivi sasa hawafanyi hivyo. Wana shughuli nyingi. Wanafanya kazi, ingawa sijui ni kazi gani. Mama yangu hakufanya kazi. Alifanya kazi nyumbani na alikuwa na kazi nyingi lakini alituangalia sisi sote. Alitusaidia pia katika kazi za shule za kufanyia nyumbani. Nilipoanza kujifunza alfabeti na kujifunza kusoma, daima aliuliza, ”Umesema nini?”, umejifunza nini leo? Ah binti yangu, unasoma vizuri”. Alicheza nasi na alitufundisha. Aliniuliza kila siku shuleni kuna nini, nimesoma kuhusu nini leo. Ilinibidi niseme na hivyo ndivyo nilivyojifunza. Alikuwa na muda na sisi. Bibi yangu pia alikuwa na muda na sisi. Wakati wa kulala alinisimulia hadithi zile zile nilizosoma. Nashukuru kwa jambo hilo, niliweza kukumbuka hadithi zote kwenye mitihani. Kilikuwa ni kipindi kizuri. Hivi sasa watoto wanatazama tamthilia kwenye runinga. Wananunua simu, za bei ghali sana, ambazo kwazo wanaweza kuitazama dunia yote, hata kama hawawezi kuiona kwa macho yao. Inahuzunisha. Maisha yamebadilika pia kuhusiana na mahusiano ya watu – yamepungua. Tumepoteza kitu fulani. Heshima kwa wazazi, kwa walimu, inabadilika. Hapo zamani ilikuwa ni haki na wajibu wa wazazi kuwatunza watoto. Kuwaangalia, kuwaambia nini ni sahihi na nini si sahihi na jinsi ya kuenenda. Hata kama mama alikuwa akifanya kazi ilimpasa kutenga muda wa mtoto kujifunza. Walikuwa wakifunzwa na mama yao, bibi yao na shangazi zao. Majirani walikuwepo karibu. Waliwaambia nini wanaweza kufanya na nini hawawezi kufanya. Kwa nini, na nini hasara yake. Hata kama mtoto angechapwa na jirani, mama yake hakusema chochote kwa sababu alitambua kwamba ni wazi alistahili adhabu. Kila mtu aliyewazunguka aliwalea watoto wao. Hata watoto wakubwa walihitaji kufundishwa. Kama wasingefundishwa, watajuaje kuheshimiana? Watajifunzaje? Wasingeweza. Maisha yanabadilika, hata hapa Zanzibar. Hivi sasa mume anafanya kazi, mke anafanya kazi. Mume hawaangalii sana watoto, si kama awali. Hapo zamani, neno ”Mwanaume” lilimaaanisha ”Mwanaume”, ilimaanisha kumtunza mke, kuwatunza watoto.
Jipe changamoto. Sahau kuhusu umri wako
Umri ni tarakimu tu. Nawajua watu ambao ni wadogo sana kwangu lakini wanaonekana wazee kunizidi. Kama unataka kuonekana kijana, unapaswa kuwa na furaha wakati wote. Unapaswa kuwa na mtazamo chanya, usifikirie mabaya, mambo hasi. Nilidhani kwamba nitakapostaafu nitapumzika, lakini sivyo. Kila wakati mwanamuziki mpya anapojiunga na bendi napaswa kumfundisha kila ala anayohitaji kupiga. Baadhi wanakuja na kusema hawawezi kujifunza kupiga ala tena kwa sababu umri wao umeenda sana. Nasema “Hapana!” nilipojifunza kupiga qanun nilikuwa na miaka 65. Hili si suala kuhusu umri, ni suala la uzima na jinsi unavyotumia akili yako. Ni kuhusu changamoto unazojiwekea. Mara ya kwanza, kama mwanamke wa kwanza kupiga qanun ilikuwa wakati wa Tamasha la Sauti za Busara. Alikuwepo Bi Kidude na vikundi vingine. Watu walisema “Usipige, watakucheka.” Lakini nilipiga kwa sababu nilikuwa nikifanya mazoezi kwa siri kwa muda mrefu. Hakuna mtu aliyekuwa akijua kuhusu hilo. Nilipopiga, nilipata pongezi nyingi sana. Watu hawapaswi kufikiria kuhusu umri wao, kwamba umri umeenda. Wanapaswa kufurahia maisha. Kama unataka kudensi – densi, kama unataka kupiga ala ya muziki – piga, kama unataka kuchora – chora, kama unataka kupika – pika. Jifurahishe mwenyewe. Kwa nini isiwe hivyo?
Yaone maisha kama zawadi
Jione wewe na kila kitu kinachokuja kwako kama zawadi. Jione kwamba wewe ni wa kipekee. Mimi bado najiona kwamba ni mtu mwenye furaha aliye na bahati ya kupata fursa ya kufanya mambo tofauti tofauti, aliye na fursa ya kuwa bora, aliye na fursa ya kujifunza. Tunapaswa kuwa na furaha na kumshukuru Mungu kwa kile tulichonacho, kwa jinsi tulivyo. Najua kwamba ninapolinganisha nyumba yangu na nyumba nyingine kubwa, yangu ni ndogo. Lakini nani kasema hivyo? Ni kubwa kwangu. Kwa sababu nina mahali pa kulala. Dada yangu anapokuja ana mahali pa kulala. Wanamuziki wanapokuja kwangu, ninayo sehemu ghorofani, ambapo mazoezi yanafanyika. Ni kubwa kwangu. Kwanini niilinganishe na nyumba nyingine za watu matajiri walionizidi? Kile nilichonacho kinanitosha. Namshukuru Mungu kwa kile nilichonacho. Watu wanazeeka kwa sababu hawafurahii kile walichonacho. Huhitaji kuwaonea watu wengine wivu. Kwenye harusi wanawake wanalitamani gauni la mwanamke mwingine, ambalo hawawezi kulimudu, lakini pembeni yao kuna mwanamke mwenye mwonekano mzuri na aliyevaa vazi la gharama nafuu tu!.
Gundua unachotaka kufanya maishani. Gundua kipaji chako
Unaponiuliza kitu gani ni cha muhimu, kwanza nitakuuliza “Unataka kufanya nini maishani?” “Kipaji chako ni nini?” Kama huwezi kukigundua, jiulize unaweza kufanya nini kwa sasa? Yawezekana unaweza kupika maandazi, kuchoma chapati. Fanya kile unachoweza kufanya leo. Mtu fulani ananiambia anaweza kuuza nguo za mitumba lakini hana mtaji. Nasema tafuta namna. Anza taratibu, “hatua kwa hatua”. Utapata chakula, huu utakuwa ni mwanzo. Kidogo kidogo utaanza kupata zaidi. Wakati mwingine mtu anakwambia uuze nguo au upike, na wewe hupendi jambo hilo. Unavutiwa, kwa mfano, na maua. Kama ndivyo, tafuta sehemu unayoweza kununua maua na fungua sehemu yako unayoweza kuuza maua. Tunapaswa kufanya kile tukipendacho maishani. Ni hasara kupoteza muda. Tunatumia muda mwingi kujifunza kitu tunachokipenda, basi tunapaswa kukifanyia kazi