
Fatma Alloo
Mwandishi wa habari
MIMI NI NANI?
Mimi ni mwanamke, mama wa mtoto mpendwa, na bibi wa watoto wake.
Ukweli wa kihistoria. Imani ya mataifa katika nguvu zao wenyewe. Imani ya Afrika katika fursa na uwezo wake yenyewe
Tunapaswa kuangalia kwenye kiini kabisa cha historia. Historia ndiyo ituambiayo wapi tulipotoka na wapi tunapokwenda. Tuna tabia ya kuharibu historia yetu, tunasema hii si historia yetu na tunataka kuibadilisha, kuiharibu historia yetu ya watu weusi. Lakini hakuna historia ya watu weusi. Historia ni moja. Historia haiwezi kubadilika. Tulikuwa koloni; Wazungu walitawala hapa. Hii ni kweli. Lakini tunapaswa kulielewa jambo hili ili kushughulikia namna ya sasa ya kufikiria ya Waafrika kwa sababu ukoloni umekuwa na madhara makubwa kwa mitizamo ya Waafrika. Hapa Afrika, neno la mzungu linathaminiwa zaidi kuliko la “ndugu mweusi”. Kama mzungu akisema kitu, kitakubaliwa kama ukweli mkamilifu, kama ndugu yako mweusi akisema kitu, hakina umuhimu. Jambo hili bado linaendelea. Linapaswa kukoma. Mfumo wa elimu wa wakoloni ulikuwa ni itikadi ya wazungu. Miaka mingi sana baada ya kukoma kwa ukoloni, vitabu vya historia bado havijabadilika mashuleni. Kwa nini hatuvibadilishi? Hivi sasa kuna kitu kimebadilika. Tunapaswa kutafakari kwa kina kuhusu Afrika, kuhusu bara letu, kuhusu sisi wenyewe na tunapaswa kujibadilisha.
Kufanya kazi pamoja kati ya wanaume na wanawake ili kujenga mahusiano mazuri. Mfumo dume unapaswa kuondoka. Kutambuliwa kwa wanawake
Tunapoongelea maendeleo ya wanawake, tunaongelea kuhusu wanawake na matatizo yanayoonekana kupitia macho yao. Wanawake wanapaswa kufahamu haki zao. Lakini ile dhamira ya kubadilika inapaswa pia kuwagusa wanaume. Wanaume nao wana shinikizo – la kuwa mwanaume. Lakini hii inamaanisha nini? Hakuna anayewasaidia. Kwa upande mwingine, wanapaswa pia kujisaidia wenyewe. Wanapaswa kuwa wanadamu iwe ni Wakristo au Waislamu. Tunapoongelea ubinadamu, dini si hoja. Kuwa binadamu kwa maana ya kumheshimu kila mtu, wakiwemo wanawake. Inapaswa kuanzia tangu utotoni kabisa, tangu umri mdogo. Tangu mwanzo mama na baba wanapaswa kuwa mfano wa namna ya kuwa na ndoa iliyo bora. Kama mwana anampiga mke wake, mama anapaswa kuikemea tabia hiyo. Hapaswi kuiruhusu tabia hiyo kwa sababu tu yule ni mwanawe. Mwanamke anamlea mwanawe walakini anamuelimisha katika mfumo dume. Tangu umri mdogo, wavulana wanaruhusiwa kucheza, jambo linalowapa burudani. Wasichana wanaambiwa wawasaidie mama zao. Kuna makatazo mengi zaidi na wajibu mwingi zaidi kwa wasichana kuliko wavulana. Huu ni mwanzo wa kuunda mtazamo na tabia. Na nani anayefanya hivi? Ni mama, si baba! Tabia zote zinazojumuisha maadili yetu zinatokea nyumbani. Hatuwezi kuliepuka hili. Kadri mfumo dume unavyodumishwa nyumbani ndivyo utakavyodumu katika jamii kwa muda mrefu. Vyombo vya habari vinapaswa pia kuzungumzia jambo hili. Makanisa na misikiti nayo inapaswa kujiunga katika hili. Tunapaswa kuzungumza kuhusu jambo hili. Tunapotazama nani anajiamini zaidi, wanaume ndiyo wanaojiamini. Mabadiliko yanapaswa kuletwa kwa pamoja, yaani wanaume na wanawake. Lakini hatuwajumuishi wanaume katika hili. Huko Kenya tayari wanaume wanaongea na wanaume wenzao kuhusu maendeleo na badiliko la tabia kuhusu wanawake. Wakisema nini si sahihi, nini si ubinadamu. Wanawake pia wanapaswa kubadilisha namna yao ya kufikiri na kuwathamini wanaume vivyo hivyo.
Wajibu wa jumuiya kwa watu wanaoishi ndani yake. Nguvu ya utamaduni wako
Hapa Zanzibar, kila mtu anamjali mwenzake. Kuna misikiti mingi sana hapa, kila wilaya ina msikiti. Kila nyumba ikipika chakula inapeleka sahani kwenye msikiti wa eneo lao, chochote kile walichopika. Hakuna mtu anayewaambia wafanye hivyo. Kila mtu asiye na makao daima atakapa chakula msikitini. Hakuna mtu atakayeweza kufa njaa. Hii ni kanuni ya msingi ambayo hakuna mtu atakayefumbua mdomo wake na kukwambia. Watu wanafanya tu wenyewe. Hii ni desturi ambayo imekuwepo kwa miaka mingi. Jambo lingine ambalo hakuna atakayekwambia ni kwamba kila eneo linakaa kikao ifikapo mfungo 15 wa Ramadhani. Majirani wote watakutana na kujadili ni mtoto gani anahitaji msaada kwa sababu siku ya Ramadhani watoto wote wanavaa nguo mpya na viatu vipya. Jamii inataka kuhakikisha ya kwamba hakuna mtoto atakayekosa vitu vipya. Anakuwa mtoto wa jumuiya. Mtoto huyu ana mama na baba lakini anakuwa wajibu wa jumuiya hiyo. Na tunajadili kuhusu kuwajibika. Na watu wanasema “Mimi natoa viatu, mimi natoa nguo”. Wanawajibika na kuwasilisha. Ukiona kila mtoto ana kitu kipya, huwezi kujua yupi ni maskini na yupi ni tajiri. Wanajumuiya wanapanga mipango yao wenyewe, hakuna serikali inayowaambia wafanye hivi. Inatokea ngazi za chini. Kuna mfumo wa maadili. Wajukuu zangu wanaposherehekea siku yao ya kuzaliwa, tunatembelea hospitali ya watoto na kuwapatia pipi. Hata kitu kidogo kinafanya maisha yawe ya furaha zaidi. Mfumo wa aina hii wa maadili ni muhimu sana na hasa kwa wanaoumudu. Mfumo huu wa maadili unamfanya mwanadamu awe binadamu.
Utambulisho binafsi. Umakini katika kukubali dhana mpya bila kutafakari
Nakumbuka harakati za ukombozi wa wanawake huko nchi za Magharibi miaka ya ‘60, ambazo pia zilitufikia na sisi. Pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanawake walinyanyapaliwa kwa sababu waliambiwa wawe kama wanaume, wavae suruali, wakate nywele zao. Nakumbuka kwamba jambo hilo lilinigusa moyo. Nilihisi si jambo ninalolitaka. Kwamba, nataka kuwa mwanamke na kubaki na huu uanamke wangu. Watetezi wengi wa Kiafrika wa haki za wanawake wamekikataa kipengele hiki cha utetezi wa haki za wanawake. Tulikwenda kivyetu. Katika suala hili, tunajivunia kwamba sisi ni wanawake. Hivi sasa naona wanawake wale wale waliohubiri mitazamo hii wakiwa wazee, wapweke sana wasio na kusudi lolote. Sasa naangalia kwa nafasi ya mzee na nachotaka kusema kwa wanawake wote, siku zinapita, mwisho wa siku unarudi nyumbani lakini kwa kitu gani? Na hicho ndicho hasa ninachomaanisha. Jibu linapaswa kupatikana kwako. Tazama nafsi yako mwenyewe, mahali kilipo chanzo cha amani yetu.
Familia. Muda kwa ajili ya familia
Hivi sasa wanawake wanafanya maamuzi kuhusu talaka kwa haraka sana. Hii si kanuni. Bado wanawake wanaowategemea wanaume kiuchumi wanabaki katika ndoa hata pale mahusiano yanapokuwa si mazuri. Wanawake wasomi na wanaojitegemea kiuchumi, naongelea kuhusu wao, wanafanya maamuzi kuhusu talaka, wakati mwingine kwa haraka sana. Kama hawana watoto, si hasara kubwa, lakini kama kuna watoto, ni jambo linalohuzunisha. Familia inahitaji muda kwa ajili yao wenyewe ili kudumisha mahusiano. Mawasiliano yamevunjika kwenye familia. Hakuna mtu mwenye muda wa kukaa chini na kuzungumza. Hawakai mezani kwa ajili ya chakula cha pamoja. Kila mtu ametingwa na shughuli. Fedha inawafanya watu wawe kama mashine. Zanzibar bado tunadumisha mahusiano ya kifamilia, kwa sababu hiki ni kisiwa kidogo.
Mfumo wa maadili ulio dhahiri. Fuata dhamiri yako
Sijui nini kimetokea kwenye jamii yetu na ni njia gani dunia imegeukia, na hivyo jambo la muhimu zaidi ni mfumo wa maadili ulio dhahiri. Huu ni mwongozo maishani mwako. Katika mfumo huu wa maadili, ni muhimu “Kutofanya kile ambacho hutaki mtu mwingine akufanyie na uishi hivyo.” Hata kama mtu amekuumiza, kumbuka usimlipizie. Ni muhimu kuwa mkarimu na kushirikiana. Huwezi kupenda mali kupita kiasi, kutengeneza dunia kulingana tu na mahitaji yako binafsi. Mwishoni mwa yote, dunia haitakulipa furaha.