bishara

Bishara Ally Masoud

Fundi wa mito 

MIMI NI NANI?

Mimi ni mama wa watoto 10. Napenda kuwasaidia watoto wangu, hata kwa wakati huu. Napenda kumsaidia kila mtu, mtu yeyote, kama nina uwezo wa kufanya hivyo. Nataka kufanya kazi kwa bidii kwa ajili yangu mwenyewe.

Fahamu wewe ni nani. Nini unataka kufanya maishani

Katika maisha ni muhimu kujua unataka kuwa nani na unataka kufanya nini. Unapaswa kujua nini cha kufanya na mwonekano wa maisha yako unapaswa kuwaje. Kwanza, unapaswa kuwajibika kwako binafsi ili uweze kuwajibika kwa wengine. 

-Je, unawezaje kugundua jambo hilo?

Inakubidi uangalie mazingira yako na kile kinachokuzunguka; wazazi, familia, majirani, jinsi wanavyoishi, jinsi mwenendo wao ulivyo na jinsi wanavyolea watoto wao. Kupitia hili tunaweza kupata mfano wa jinsi hasa ya kulea watoto wetu, jinsi ya kuenenda na kufahamiana. Nimetokea mbali kabla ya kufika nilipo leo maishani. Niliolewa, mume wangu hakuwa mwema kwangu na watoto wangu; maisha yalikuwa ya huzuni. Nikaanza kupata mawazo haya: Kwa nini namruhusu aniumize mimi na watoto wangu? Nikaamua kwamba nitaanza kulifanyia kazi suala la kujitegemea na kuweza kununua chakula changu mimi mwenyewe. Nilianza na biashara ndogo ya kuuza chakula. Hili lilikuwa jawabu langu la kujimudu mwenyewe. Nikaanza kufanya jambo ili nibadilishe hali yangu na nijibadilishe mimi binafsi. Daima nilitafuta fursa mpya. Unapozitafuta, daima zitakuja kwako, daima utazipata baadhi, inakubidi tu uwe macho na uzitafute. 

Sayansi

Watoto wanapaswa kupewa mambo matatu: maadili, chakula na elimu. Kujifunza ni jambo muhimu zaidi. Ukijifunza utapata maarifa na utaweza kuyajenga maisha yako mwenyewe na ya watoto wako. 

Usigombane 

Kuwa mkarimu kwa mtu asiyekuwa mkarimu kwako. Hii ni kanuni yetu. Nimewafundisha watoto wangu kuishi kwa mapatano na watu wengine, kwamba waishi kwa kupatana, kwamba wawe watu wema, kwamba waheshimu watu wengine. Kwamba wanapokuwa kwenye mzozo na mtu mwingine, kwamba watafute suluhu kwa kutumia hekima, ila wasigombane. Kwamba daima wawe na mawazo chanya na mwenendo mzuri; hivyo ndivyo nilivyowafundisha watoto wangu. Pale mtu fulani anapoanzisha ugomvi na mwingine akimrudishia – kwa kugombana – hakuna nafasi ya suluhu, isipokuwa ukatili zaidi na mateso zaidi. Mwenendo huu utazaa tu chuki, ukatili na mateso kwa pande zote mbili. Pale watoto wanapokua pamoja na watoto wa familia nyingine au pamoja na watoto wa majirani au marafiki na mmoja wao akaanza kuwapiga wengine, kila mtu wa karibu naye ataanza kupigana. Haitamletea mtu yeyote faida. Pale baadhi ya watoto kwenye jumuiya wanapoanza kuwa na mwenendo mbaya, kama kuvuta sigara, kunywa pombe, na jamii ikaliangalia tu jambo hili, hakuna jema litakalotokana na jambo hili.

Kuwa mwema kwa wengine

Hii ni kanuni inayotuongoza kwenye jumuiya yetu. Mimi ni mkarimu kwa mtu mwingine na mtu huyu ni mkarimu kwangu. Watu wengine wanafanya hivyo hivyo na kwa njia hii jumuiya yote inaundwa na watu walio wema na wanaokirimiana. Hii inamaanisha kwamba kama mtu fulani ni mwema na mcheshi, mtu mwingine naye ataonesha uchangamfu. Hata kama mtu ni mwovu na anafanya mambo mabaya, tulia na uwe mwema. 

Baki kwenye ardhi yako, nchini mwako

Ningependa kuwaambia vijana kwamba maisha ni hapa hapa; kwamba hawapaswi kwenda Ulaya ili kutafuta maisha yenye furaha. Wanaweza kubaki na kufanya kazi hapa, kujenga miji yao hapa, hapa ndipo patakapowalisha. Hapa ni nyumbani kwao. Hii ni ardhi itakayowapa kazi, wanaweza kupata kazi hapa na kufikia malengo yao. Jawabu si Ulaya; jawabu lipo mahali ilipo nchi yao. 

Fedha inaleta furaha, lakini kama tu inatokana na kazi yako binafsi 

Fedha peke yake bila kuitolea jasho haileti furaha. Ningependa kuwaambia watu kwamba thamani ya maisha ni kutafuta kazi, kufanya kazi, kujipatia kipato chako wenyewe na kutafuta kitu kitakachokupa raha maishani. Na hilo ndilo linalonipa mimi raha. Ukweli kwamba nafanya kazi kwa bidii, najipatia kipato changu mwenyewe na kwamba sihitaji kumwomba mtu yeyote pesa. Napenda kuja sehemu yangu ya kazi na wakati mwingine nashinda hapa kutwa nzima. Kisha narudi nyumbani, na kutafakari mambo mengi, lakini huwa najiuliza, “Ni vitu gani vingine naweza kufanya kwa sasa? Labda nitengeneze sharubati; watoto wanaorudi kutoka shule wanaweza kununua kwa Sh 200 – 300.” Nakusanya vichenji-chenji na nafurahi kwamba vinaongezeka. Naweza kuifanya hii hata nyumbani; naendelea kufanya kazi kadri niwezavyo.

Join us … travelling and discovering culture, people and yourself