ally

Ally Abdallach Duhi

Mwanapatholojia

MIMI NI NANI?

Nina miaka 80. Mimi ni mwanaume. Nimeshaona mambo mengi sana maishani mwangu. Nilizaliwa kwenye kijiji maskini sana. Nilipata elimu Zanzibar, kisha nikaenda shule ya utabibu huko Urusi. Nilisoma Kiev. Nilifunga ndoa hapa Zanzibar, mke wangu alikuwa Mkristo. Mimi ni kama watu wengine. Nina akili, utashi, naweza kufanya maamuzi mwenyewe; kile nachotaka na kile nisichotaka. Naweza kushirikiana mambo mengine, chakula, mawazo. Naweza kuongea, naweza kufanya mambo mengi kama mwanadamu anayeishi, ambaye bado hajafa. Nitakapokufa nitapoteza kila kitu. Ninayo furaha ya kuweza kuongea na wewe na kwamba unasikiliza kile nisemacho. Nina furaha. 

Uwezekano wa kuwa mwanadamu

Thamani ni kuwa mtu aliyeumbwa na Mungu kutoka udongo mweupe, mwekundu na mweusi. Hii ndiyo sababu baadhi yetu ni weupe, baadhi ni wekundu na wengine ni weusi. Wazungu ni weupe na Waafrika ni weusi. Tuko tofauti kwa sababu tu ya jua, miale yake inatufanya tuwe tofauti. Unapaswa kutambua inamaanisha nini kuwa mwanadamu. Kama watu, tuna utashi wenye ukomo wa kuelewa kila kitu. Bila ya uhai, bila ya kuwa mwanadamu hai, hutakuwa na thamani. Mungu aliwaumba Adamu na Hawa. Mwanamke ni muhimu sana, ana jukumu muhimu zaidi la kulitimiliza, yeye ana wajibu zaidi kwa kuwa anapaswa kulea watoto wake. Mwanaume anatengenenza mbegu milioni 100 zinazoenda kupevusha yai moja na ni mbegu moja tu inayofanikiwa. Hili ni jambo la ajabu sana! Ndiyo maana kila mwanadamu ni wa kipekee. Tunapaswa pia kukumbuka nini ni muhimu kwa miili yetu. Maji ni muhimu na jua ni muhimu. Ulimwengu ni mwerevu sana.

Kazi

Maishani ni muhimu kufanya kazi, tunashukuru kwa hilo kwamba tunatengeneza thamani yetu. Wakati mwingine najiuliza kwa nini Mungu bado hajanipa uhuru, kwa nini amenipa maisha marefu. Lazima nifanye kazi, napaswa kwenda nje kwenye jua, napaswa kutembea kwenye ufukwe, napaswa kufanya kitu au kutengeneza kitu. Hii ni thamani ya mwanadamu na asili yake. Huwezi kuwa na thamani bila ya kazi. Kama ilivyo bila chakula hutakuwa na thamani. Maisha ni kazi. Pumzika, cheka na fanya kazi, pumzika na fanya kazi tena. Kadri utakavyokuwa na afya, unapaswa kufanya kazi. Vinginevyo, hutakuwa na afya. Unapaswa kufanya kazi ili kutengeneza, ili kusaidia kutengeneza maisha. Tengeneza maisha kwanza kwa ajili yako mwenyewe na kisha kwa ajili ya wengine, kwa kila kitu kinachokuzunguka. Lakini kama kazi yako haikufanyi uridhike, anza kufanya kitu kingine. 

Maisha

Kuishi ni jambo muhimu zaidi maishani, jambo muhimu zaidi ni kuishi. Usife, ishi. Ninachoamini ni kwamba maisha ni muhumu sana na yana thamani sana lakini unapaswa kuyaelewa. Kuelewa maisha kunamaanisha kuelewa kwamba unapaswa kuyafuata, kuyafurahia na kuwa na amani. Maisha ni kuzaliwa na kufa. Kama uko hai unapaswa kufurahia jambo hilo. Na kama unafurahia, utaishi maisha marefu. Wakati mwingine mnasema: ”Ukiongea sana utakuwa na maisha mafupi” (kicheko). Lakini kama ukiongea, ukiongea sana, unaweza kuelewa zaidi. Inategemea wewe na maadili yako. Kwa sasa nimestaafu. Maisha ni ya thamani kubwa kwangu na ni starehe kwangu. Starehe inatokana na uchaguzi binafsi. Uradhi, furaha ni mambo binafsi sana na inategemeana na mtu. Jambo lililo zuri kwako, si lazima liwe zuri kwangu. Hii ni fasili ya kile tunachokiita kuridhika, furaha – hakuna fasili moja. Kwa mimi, kinachonipa kuridhika kwa sasa ni utulivu kwamba naweza kulala, nina chakula. Naweza kukutana na watu wema. Naweza kupata kila kitu kinachohitajika kwangu na kinachonipa faraja. Hivyo tu. Sihitaji chochote kutoka kwa mtu. Nina nyumba, nina watoto. Kwa sasa nahitaji maisha tu. Nahitaji maisha ili nifurahi, sihitaji matatizo tena. Chukua kila kitu upewacho na maisha ambacho kinakupa maisha mazuri. 

– Wakati mwingine kitu fulani kinatupa raha lakini kinatuangamiza.

– Akili yako inapaswa kutafuta jibu zuri. Lakini wakati mwingine hujui kipi ni kizuri na kipi si kizuri. Basi fuata hisia zako, moyo wako na utaendelea kuwa hai.

Dunia

Dunia ni muhimu sana. Dunia ni ya thamani ya kipekee, lakini unapaswa kuielewa. 

Mabadiliko

Kupigana ni aina ya maisha. Mapinduzi, mapinduzi ya kila mara, yanabadilisha maisha. Baadhi wanasema kwamba mabadiliko yanaleta maisha bora, baadhi wanasema yanaleta maisha magumu, lakini daima ni kuhusu mabadiliko. Akili yetu inabadilika pia. Kamwe hakuna udumifu. 

– Na je, nini ni cha kudumu?

Kwa maoni yangu hakuna udumifu. Kila kitu kinabadilika. Maisha yanapaswa kubadilka. Kila siku ni tofauti. Juzi, jana, leo kesho, kesho kutwa. Hata siku moja ni tofauti – mvua imetoka kunyesha na sasa jua linawaka. Maisha ni mabadiliko yaliyo endelevu. Tumeumbwa ili tuumbe, tuumbe kila mara. Akili yetu inafanya kazi wakati wote, hata tukiwa tumelala, akili inafanya kazi, inaota. Kuna kitu kinabadilika kila wakati. Mungu alijiumba yeye mwenyewe ili mchakato huu uwe endelevu. Mabadiliko ni njia bora maishani. Mabadiliko ni njia bora kwa maisha. Kama bado upo sehemu moja huwezi kuishi maisha bora au yenye maadili. Maadili mema na maadili mabovu, kama nilivyosema, yanahusiana. Kila kitu kinahusiana. Kitu ambacho ni kizuri kwangu si kizuri kwa mwingine. 

Haijulikani

Si mwanapatholojia wala mtu yeyote yule ajuaye nini kipo baada ya kifo na hiyo pia ni thamani maishani. Niliamua kuwa mwanapatholojia kwa sababu wazo lilikuwa kwamba, nilipokuwa nikisoma kozi hii, nitaweza kupata jibu la swali la nini kipo baada ya kifo. Katika kipindi cha kazi yangu, nimechunguza miili zaidi ya 1,500. Miili tofauti tofauti ya watu waliopoteza maisha yao kwenye matukio mbalimbali, lakini miili yao haikusema chochote. Ili kupata jibu unapaswa kufanya kazi kwa bidii. Ili kujua nini kipo baada ya kifo unapaswa kupoteza maisha. Unapaswa kubadilika. Ndiyo maana dunia inabadilika kila mara kwa sababu inatafuta majibu ya maswali mbalimbali. Maisha lazima yabadilike kila mara. Lakini watu wanaogopa mabadiliko. Watu wanaogopa mabadiliko kwa sababu Mungu aliwapa machale, udhanifu na hisia. Kila mtu anaogopa jambo hili. Lakini hata kama wanaogopa, bado linakuja, wanalihisi. Kifo hakina faida kwa sababu watu wanakiogopa. Tangu mwanzo kabisa, tunapozaliwa, tunajua kwamba tutakufa, lakini bado hatutaki kufa. Mimi pia, ningependa kuzaliwa tena (kicheko).

Usiharakishe kufanya chaguzi. Muda. Marudio. 

Ili kufanya uchaguzi mzuri unapaswa kuwa na subira, usiharakishe, subiri, jipe muda. Kisha kila kitu kitakuja kwako moja kwa moja. Kama una haraka, jibu litakuja kwako lakini si la kweli. Hata mimi, ilinibidi nitafakari kidogo kabla sijajibu swali lako. Kabla sijajibu, nilikuuliza mara mbili ili kuona kama nimelielewa vizuri. Unapaswa kuwa na uhakika. Kama ilivyo katika maisha. Kama unataka kufanikiwa, unapaswa kuwa na uhakika. Usiharakishe. Bora utende kosa na kulirudia. Marudio si jambo baya. Marudio yanamaanisha kujisahihisha, yanamaanisha kuwa bora zaidi. Hii ni thamani maishani. Kama hurudii kitu fulani, hutoweza kupata thamani yake.

-Je, unawaambia nini watu wanaoogopa kufanya uchaguzi? Wafanye nini?

Wasubiri. Wasubiri mpaka waone hasa kama wanaogopa au la. Usiharakishe kujibu. Usirukie jambo fulani. Ngoja kwanza. Kisha utajua. Akili yako itakupa jibu. Akili itafanya kazi na kutafuta jibu. Muda utakupa jibu.

Join us … travelling and discovering culture, people and yourself