DECALOG_TABLICE13-1

Prof. Abdul Sheriff

mwanahistoria

MIMI NI NANI?

Nazungumza Kiswahili. Mimi ni Mzanzibari mwenye asili ya Kihindu. 

Wajibu kwa maisha yako binafsi

Kutengeneza wasifu wako na maisha yako kunakutegemea wewe. Hakutegemei kitu kinachokutengeneza wewe, au fikra yoyote ile au maisha katika kipindi mahsusi cha kihistoria. Inategemea na wewe. 

Kuwa halisi. Jigundue na ishi kwa amani na uhalisia wako hasa

Ni muhimu kwangu kuwa na uhalisia. Usijifanye kuwa mtu asiye wewe, usikubali pendekezo lolote kuhusu nani unapaswa kuwa, bali jigundue na ishi kwa kiwango bora cha mtu huyo – ambaye ni wewe hasa. Nilipoishi nchi za Magharibi, baadhi ya rafiki zangu baada ya kuwasili Marekani walibadilisha majina yao, wakitaka kufanana na mazingira mapya. Lakini je, hii ni sura yao halisi? Je, wameukimbia utaifa wao kwa sababu ya jambo hilo? Je, watakuwa halisi? Maana kwa hakika ulivyo wewe ni matokeo ya mchanganyiko wa tamaduni nyingi, ambazo ni nzuri na mbaya, lakini kitu cha muhimu zaidi ni kwamba unaishi kwa maadili muhimu muhimu zaidi maishani mwako. 

Kuyafahamu yaliyopita yanayoishi katika wakati uliopo

Kuna mtu aliniambia ”Profesa unaishi katika wakati uliopita”. Hapana. Mimi ni mwanahistoria ninayeyafahamu yaliyopita lakini naishi katika wakati wa sasa. Nadhani kwamba hili ndilo moja ya matatizo ya kizazi kipya, kutoelewa kati ya historia na wakati uliopita. Vijana hawatafakari kuhusu siku za nyuma. Baadhi ya watu hulielewa hii tu wanapokuwa watu wazima. Unapokuwa mtu mzima unaanza kuelewa mambo yaliyo magumu kwa watu wote. Huu ndiyo mwanzo wa kuanza kujiuliza unatokea wapi? Mahali unapotokea ni mapito yako yanayobainisha wewe ni nani? Bibi yako alisema nini? Ulifikaje hapa ulipo sasa? Ulikuwa na makuzi gani katika jumuiya yako ambayo unaishi humo hivi sasa? Jumuiya yako inatokea wapi? Kulitokea nini katika siku za nyuma? Kama unaelewa jambo hili, utaelewa siku zako za nyuma zinamaanisha nini. Si kuongelea siku za nyuma zilikuwaje lakini kuelewa matokeo yake katika wakati wa sasa. 

Kuheshimu jumuiya yetu na watu wanaotuzunguka

Huko Morocco, rafiki wa baba yangu aliyekuwa akiishi huko aliniambia alikuwa na misha mazuri. Kila siku alikuwa anaweza kula nyama pamoja na familia yote. Lakini jirani zake wanakula mboga za majani kila siku, wananunua nyama siku moja tu kwa wiki. Anapokwenda sokoni ananunua nyama kila siku lakini anaificha chini kabisa ya kikapu. Kisha ananunua mboga za majani na kuziweka juu ya kikapu. Anaporudi nyumbani kila mtu anaona amenunua mboga za majani. Nikawaza, hii ni dhana ya kuishi pamoja katika jamii. Je, ujirani unamaanisha nini? Unazungukwa na nyumba 40, ambapo kuna familia 40, ndani yao kuna familia na watu ambao hukuwachagua wewe. Kuielewa jumuiya yako mwenyewe, kuuelewa utamaduni wako mwenyewe ni jambo la muhimu. Na kuelewa mara kwa mara mahusiano ya kimwingiliano. Huwezi kuishi nje ya utamaduni iliyo tofauti: maskini na matajiri, wanawake na wanaume, weupe na weusi, daima kutakuwa na tofauti fulani.  Aina hii ya kuheshimu uanuwai yawezekana imetokana na mwongozo wa kiroho. Sidhani kama inatokana na sababu za kiasili, ingawa naweza kutokuwa sahihi katika hili. 

Kuelewa kile tufanyacho. Kuelewa kiini cha dini. Si tu kufanya desturi za nje

Swala haina maana kwangu, lakini si kwa kila mtu. Kuna wakati fulani niliongea na rafiki yangu mpendwa, alikuwa na miaka 100. Aliniuliza kwa nini sifanyi swala kila siku, nikamwambia ninapofanya swala napata hisia fulani tu ndani yangu, lakini sihisi kiunganisho na moyo wangu, imani yangu. Swala peke yake, bila ya kuhamishia maadili yake katika maisha ya kila siku, ni jambo lisilo na maana kwangu. Akajibu “Sawa”. Hakujaribu kuniongoa. Dini, Uislamu ni sehemu ya maisha yangu na kwa ukweli huu huwa najaribu kuachana na njia zangu za kidunia. Nachoamini katika maisha yangu ni utajiri wa kihistoria au mifumo inayoongoza historia. Hata kama unaielewa dini, huwezi kuelewa kwa undani hasa maana yake. Kwa mfano, swala. Yawezekana hujui kwa nini unaswali. Hivi sasa kuna desturi fulani imekuja, desturi ya muda mfupi ya tabia fulani hivi. Hasa vijana, kila siku wanatumiana ujumbe mfupi kupitia “WhatsApp” na “Messenger” ili kuhabarishana baadhi ya taarifa, matangazo, ambavyo ni vile vile wakati wote. Kwa wengi wao, jambo hili linakuwa ashiki ya muda mfupi. Iiwapo dini zinaundwa kwa namna kama hii, basi tunatengeneza watu wanaokoma kufikiri. Kama tunatuma ujumbe mfupi kwa wengine ilimradi tu tumeutuma, hatufikirii hata ni kitu gani tunachokituma, maana yake, nini mpokeaji anachoweza kukisoma, tunataka kumwambia nini? Ndiyo maana ni muhimu kuelewa unafanya swala kwa sababu gani? Ni rahisi kufungua kitabu kile kile kila siku kwenye sura tofauti, lakini kikawa kinakushughulisha tu. Dini inaweka mkazo zaidi katika swala. Hata kama usipoyaelewa maneno yote, unayarudia tu hivyo hivyo. Lakini hata kama unayaelewa na kuyarudia kila mara, unapoteza uelewa wa kile unachosoma. Ni muhimu wakati wote kuelewa kile unachokifanya. Kila siku. Hata kama huielewi sentensi fulani leo, unaweza kuielewa kesho. Kuelewa ni changamoto lakini jaribu kukabiliana nayo. Kwa upande wangu, dini inafundisha maisha, inakufundisha kuwa na amani katika nafsi yako mwenyewe. Kama dini inakufundisha, inamaanisha kwamba inakuongoza hakika. Sayansi ya dini, mbali na yote, ni sayansi ya namna ya kuwa binadamu. Mungu anakutaka ujigundue wewe mwenyewe kupitia mahusiano na mwanadamu mwingine. Kama unatumia maisha yako yote kuswali msikitini, utajihisi vizuri, lakini Mungu atahisi kwamba umeyapoteza maisha yako kwa sababu hujapata maarifa, hujajaribu kumjua Mungu kupitia mwanadamu mwingine. Na si tu kupitia mwanadamu mwingine, lakini pia kupitia mahusiano pamoja na wanyama, mimea na kila kitu kinachtuzunguka. Ni muhimu jinsi unavyowatendea wanyama, mimea na kila kitu kinachokuzunguka. Hicho ndicho kiini cha dini.

Mahusiano na Mungu na mwanadamu. Tahadhari katika kuhukumu. Unyeti 

Baada ya sala, Imam aliketi mlangoni pa Msikiti. Mlevi mmoja akaja na kutaka kuingia msikitini. Vijana wa kiume wakaanza kupaza sauti kwamba haruhusiwi kuingia ndani kwa kuwa alikuwa amelewa. Wale vijana walitaka kumfukuzia mbali. Imam akasema “Hapana”, na akawauliza “Mtu huyu anataka kuingia ndani ili afanye swala, kwa nini mnamzuia? Kwa sababu amelewa? Je, maadili ya Kiislamu ndiyo yanasema hivyo? Je, hii ndiyo sababu ya kutomruhusu aingie ndani? Mruhusuni aingie ndani.” Akaingia ndani lakini akamwomba Imam amsaidie kufanya swala. Iman akamsogelea na yule mtu akafuatisha kila hatua aliyofanya Imam. Alihitaji msaada wa kugusisha paji la uso wake sakafuni. Alipofanya hivyo, hakuinuka tena. Swala ilipomalizika, watu wakamfuata, wakidhani kwamba amelala usingizi. Alikuwa amekufa! Mtu huyu alikuja ili afie Msikitini! Hili ni somo muhimu sana. 

Join us … travelling and discovering culture, people and yourself